REAL MADRID MABIGWA WAPYA WA UEFA CHAMPIONS LEAGUE 2017
Klabu ya Real Madrid ya Uhispania imeicharaza Juventus ya Italia 4-1 na kushinda Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mreno Cristiano Ronaldo alifunga mabao mawili, la kwanza kwake na klabu dakika ya 20 na lake la pili dakika ya 64 kutoka kwa krosi ya Luka Modric.
Casemiro aliwafungia Real bao lao la pili dakika ya 61 kabla ya Marco Asensio kukamilisha ushindi wao dakika ya 90 kwa bao lao la nne.
Juventus, waliokuwa wameanza vyema mechi hiyo wakikuwa wamekomboa bao la kwanza la Ronaldo dakika ya 27 kupitia Mario Mandzukic na kufanya mambo kuwa sare wakati wa mapumziko lakini kipindi cha pili mawimbi yaliwageuka.
Nguvu mpya wao Juan Cuadrado alipewa kadi ya pili ya manjano dakika ya 84, baada ya kukaa uwanjani dakika 18 pekee.
Gareth Bale aliingia kwenye mechi hiyo kama nguvu mpya dakika ya 77, mara yake ya kwanza kuchezeshwa mechi ya ushindani tangu 23 Aprili.
Real Madrid wamefanikiwa kuwa klabu ya kwanza tangu AC Milan (1989, 1990) kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya misimu miwili mfululizo, na ni mara yao ya 12 kushinda kombe hilo.
Mwaka huu ni mara ya tatu kwa Real Madrid kufika fainali katika misimu minne.
Juve ndiyo klabu pekee ambayo ilikuwa haijashindwa mechi yoyote msimu huu Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, klabu ya kwanza tangu Atletico Madrid mwaka 2013/14 kufika fainali bila kushindwa.
Real Madrid nao walikuwa wamefunga kila mechi kati ya mechi 12 walizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu.
Kushindwa kwa Juventus ni pigo kubwa kwa nahodha wao, mlinda lango Gianluigi Buffon, 39, ambaye hajawahi kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Kabla ya mechi, alikuwa amesema ushindi ungekuwa na maana kubwa sana kwake.
Comments
Post a Comment