UEFA FAINALI: BINGWA KATI YA REAL MADRID NA JUVENTUS KUFAHAMIKA LEO
Mkufunzi mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane anakabiliwa na kizungumkuti cha kuamua nani kati ya Gareth Bale na Isco atacheza katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya leo.
Bale hajacheza tangu 23 Aprili lakini sasa yuko sawa kucheza.
Isco, ambaye alijaza pengo lake naye amekuwa akicheza vyema sana na amefunga mabao matano katika mechi nane walizocheza hivi karibuni.
"Wote wawili ni wachezaji muhimu sana na kila mmoja anaweza kutoa maoni yake lakini hilo halitaniathiri," Zidane amesema.
Mkufunzi wa Juventus Max Allegri wachezaji wake wote pia wako sawa kucheza.
Gianluigi Buffon, Giorgio Chellini, Alex Sandro, Mario Mandzukic na Leonardo Bonucci walipumzishwa mechi ya mwisho ya Juve katika Serie A dhidi ya Bologna Jumamosi iliyopita.
Gianluigi Buffon, 39, atakuwa nahodha wa Juve katika mechi hiyo itakayochezewa Cardiff.
Buffon hajawahi kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
"Itakuwa na maana kubwa sana kwangu," anasema mchezaji huyo, ambaye amechezea Italia mechi 168.
"Itakuwa siku ya furaha zaidi kwangu katika maisha yangu ya uchezaji, pamoja na Kombe la Dunia - kwa sababu itakuwa ni kama zawadi, baada ya safari ngumu yenye dhiki na visiki na bidii."
Juventus walilaza Monaco 4-1 na kufika fainali kwa mara ya pili katika misimu mitatu.
Real Madrid nao waliwatoa Atletico kwa ushindi wa jumla wa 4-2.
Ronaldo, ambaye alifunga penalti ya ushindi fainali msimu uliopita, anasema amepumzika vya kutosha na ako makini kabisa.
"Mwisho wa msimu ni muhimu sana," anasema.
Ronaldo alifikia magoli 400 ambayo amefungia Real msimu wa sasa, pamoja na mabao 100 Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Hii itakuwa mechi ya 19 kwa klabu hizo mbili kukutana, mechi zote zikiwa katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya.
Klabu hizo ndizo zilizokutana mara nyingi kabisa historia ya michuano hiyo, baada ya Bayern dhidi ya Real Madrid (24).
Juventus na Real Madrid, kila mmoja ameshinda mechi nane kati ya hizo, mechi mbili zikimalizika kwa sare.
Mechi yao pekee kukutana fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Real walishinda 1-0 mwaka 1998 kupitia bao la Pedrag Mijatovic.
Juventus wameshinda mara mbili pekee kati ya fainali nane walizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya. Walishindwa fainali nne walizocheza karibuni zaidi mwaka 1997, 1998, 2003 na 2015.
Real Madrid wanapigania kuwa klabu ya kwanza tangu AC Milan (1989, 1990) kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya misimu miwili mfululizo.
Mwaka huu ni mara ya tatu kwa Real Madrid kufika fainali katika misimu minne.
Juve ndiyo klabu pekee ambayo haijashindwa mechi yoyote msimu huu Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, klabu ya kwanza tangu Atletico Madrid mwaka 2013/14 kufika fainali bila kushindwa.
Real Madrid nao wamefunga kila mechi kati ya mechi 12 walizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu.
Comments
Post a Comment